Kwa mujibu wa idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi, miongoni mwa wanazuoni wa Iraq wanaoishi katika mji mtakatifu wa Karbala, ametoa shukrani zake kwa ushirikiano wa karibu na uhusiano wa kindugu baina ya wananchi wa Iraq na Iran ambao umeshuhudiwa katika miongo miwili iliyopita; uhusiano ambao umejitokeza wazi katika nyakati za misukosuko na katika hali ngumu, na katika hatua nyingi umefikia hata kiwango cha ushirikiano wa watoto wa nchi moja.
Katika darsa yake ya kila wiki ya maadili anayoitoa katika ofisi yake mjini Karbala Tukufu, alikosoa baadhi ya maamuzi na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Iraq ambazo, kwa mtazamo wake, ziko mbali na mwelekeo wa wananchi na Marja’iyya; miongoni mwa mambo hayo ni kuweka vizuizi katika safari za mazuwari wa Imam Husain (a.s.) na maeneo mengine matakatifu ya ziara nchini Iraq, pamoja na kufunga anga au njia za kuingia mbele ya wale wanaokuja kufanya ziara, jambo ambalo limefanywa kwa kujibu vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi jirani na taifa la Kiislamu.
Alieleza kwamba; wale wanaokuja Iraq kupitia Iran si wote ni Wairani, bali miongoni mwao wapo mazuwari kutoka mataifa na nchi mbalimbali ambao wanafuata lengo moja la kidini, yaani kuzuru maeneo matakatifu na kutekeleza ibada na alama za imani. Kwa hiyo, kushughulikia safari za mazuwari hawa kunapaswa kuzingatia asili ya lengo lao la kidini, na si tofauti na misimamo ya kisiasa baina ya nchi.
Ayatullah Mudarrisi alifafanua: Jambo hili kwa upande huu linafanana na safari ya Waislamu kwa ajili ya kutekeleza faradhi ya Hija; kwa sababu hata wakati wa kuwepo migogoro na tofauti za kisiasa baina ya nchi na serikali, haikukubalika kwamba tofauti hizo zitumike kama sababu ya kuwazuia mahujaji kufika katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu, au kuzuia ndege, mabasi na vyombo vya usafiri vinavyowapeleka kutekeleza ibada zao.
Alisisitiza: Kuingiza ibada za kidini na safari za mahujaji katika migogoro ya kisiasa, kuwazuia watu kufika au kuwawekea vikwazo katika njia ya kuelekea kwenye maeneo matakatifu, haipaswi kuwa chombo cha shinikizo baina ya nchi; kwa sababu jambo hili linadhuru haki ya watu ya kutekeleza ibada zao za kidini na linaweza, kwa vitendo, kugeuka kuwa upinzani dhidi ya dini na ibada zake.
Aliongeza: Kinachotarajiwa kutoka kwa viongozi wa Iraq, badala ya kuweka vizuizi kwenye safari za mazuwari, ni kufanya juhudi za kurahisisha kuingia kwao kupitia njia mbalimbali za anga na nchi kavu, na kuendeleza viwanja vya ndege, barabara, vituo vya mipakani na miundombinu, kwa namna itakayolingana na makumi ya mamilioni ya mazuwari na wasafiri ambao kila mwaka wanaifanya Iraq na maeneo yake matakatifu kuwa kituo cha safari zao.
Mwanazuoni huyo wa Iraq alisema: Maadui wa Umma daima hutafuta njia ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko baina ya wananchi wa eneo hili na kukata madaraja ya mawasiliano, ushirikiano na mshikamano baina yao. Alionya dhidi ya kuitikia shinikizo na maagizo yanayolenga upande huo; kwa sababu hatua kama hizo zinatoa fursa ya kutawala ardhi za Waislamu na kudhoofisha mataifa yao.
Mwisho, alisisitiza ulazima wa kuhifadhi uhusiano wa kindugu baina ya mataifa ya Kiislamu na kutoruhusu tofauti na maslahi ya kisiasa ya muda mfupi kukata njia za mawasiliano baina yao au kuwazuia Waumini kutekeleza ibada na kuzuru maeneo matakatifu.
Maoni yako